ImageNdanda Kosovo kuzikwa leo
Leo ni Siku ya Maziko ya Mwanamuziki maarufu, Ndanda Kosovo, mwenye asili ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ambaye aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi nchini Tanzania alikokuwa anafanya Shughuli zake za muziki.
Balozi wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Jean Pierre Mutamba akiongozana na viongozi kadhaa wa Tanzania watashiriki tukio la kutoa heshima kwa kuwa Msanii huyo aliutangaza Muziki wa Congo Duniani na alichangia kukuza Muziki wa Dansi nchini Tanzania.
Ndanda akiwa jijini Dar es Salaam Tanzania aliwika na Bendi ya FM Academia International akiwa na vijana wenzake waliokuwa na asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Baadaye Ndanda alitoka FM Academia International akaanzisha Bendi ya Stono Musica akiita Wajelajela Original. Na hapo alitamba sana na kibao chao cha JELA ambacho alikitunga mara baada ya kutoka Jela pale ambapo yeye na wenzake walikuwa wamekamatwa kwa kuingia na kufanya kazi nchini Tanzania bila vibali.
Nyimbo zake nyingine zilizotamba ni pamoja na Binadamu, Chini ya Ulinzi, Chozi la Mnyonge na nyingine nyingi pamoja na vionjo kama Kidedea na Kaokota Big G.
Miaka kadhaa baadaye Ndanda aliachana na Stono Musica akahamia Marekani kwa shughuli za kimuziki kabla ya kurejea Tanzania na kuanzisha Kundi la Watoto wa Tembo ambalo hata hivyo aliachana nalo na kuwa Msanii wa kujitegemea.
Habari kutoka BBC swahili
No comments:
Post a Comment